Envaya
Maeneo ya ukurasa huu yametafsiriwa toka (unknown language) kwa Kiswahili. Ona asili · Hariri tafsiri

MED Yaomba Wastaafu Kufundisha kwa Mikataba.

Asasi ya Marafiki wa Elimu Dodoma MED imemwomba Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ushari ya Wilaya (DCC) Bw. John Tuppa; kuishauri kamati yake ili iwatumie walimu wastaafu kufundisha shule za sekondari za kata.

Barua ya MED yenye maombi hayo iliwasilishwa kwa Mkuu wa Wilaya kwa lengo la kusaidia kupunguza tatizo la uhaba wa walimu katika shule za kata katika Wilaya ya Dodoma.

Kwa mujibu wa barua hiyo; MED imemuomba Bw. Tuppa kuwatumia walimu wastaafu kufundisha katika shule za kata ambazo wastaafu hao wanaishi badala ya kuendelea kuwasubiri vijana wadogo wanaohitimu masomo na kwenda kufundisha kwenye shule hizo bila kuzaa matunda tarajiwa.

Barua hiyo ilieleza kuwa; licha ya nia ya serikali kuwatumia wahitimu wa kidato cha sita kuziba pengom la walimu; wahitimu hao wamekuwa wakituhumiwa kuwa sehemu ya chanzo cha ongezeko la mimba kwa wanafunzi wa shuleni wanazo fundisha.

Baadhi ya wadau wameipongeza MED kwa hatua hiyo ya uthubutu waliyo ichukua  kwa Mkuu wa Wilaya na kuongeza kuwa; wastaafu wengi wenye taaluma ya ualimu wana maadili ya kazi hiyo hivyo wanaweza  kusaidia sana kupunguza tatizo la uhaba wa walimu kwenye shule za kata kama wastaafu hao watatumika ipasavyo na kupewa stahili zao.

Mratibu wa MED Bw. Davis Makundi amekiri kumwandikia Mkuu wa Wilaya barua hiyo na kusema; hiyo ni haki ya msingi kwa mtu binafsi, taasisi au kikundi chochote cha kijamii kwani barua hiyo ni ya kumshauri na si ya amri kwa kiongozi huyo wa Wilaya.

 

Wenye Ulemavu Waomba Msaada wa Vifaa.

Watu wenye changamoto za ulemavu wamewaomba wanasiasa kuwasaidia kupata nyenzo mbalimbali kwa ajili ya shughuli zao za kila siku.

Wakiongea  kwa nyakati tofauti na MED wanachama wa Chama Cha Viziwi Tanzania (CHAVITA) tawi la Dodoma wamesema; wanasiasa wana nafasi nzuri ya kutetea haki za walemavu kama kweli wakidhamiria kufanya hivyo.

Mwenyekiti wa CHAVITA tawi la Kondoa Bw. Mustafa Shabani amesema watu wenye ulemavu wana changamoto ningi za kimaendeleo zinazo sababishwa na ulemavu wao. Alisema kwamba wao kama watu wengne wanahitaji kupata taarifalakini hawazipati kwa usahihi kutokana na wao kukosa vifaa maalum vya kuongeza usikivu au wakalimani.

Naye Bw. Ally Jumanne ambaye ni katibu wa chama hicho alisema ni vema wanasiasa wakasaida kuishawishi serikali ijali haki na mahitaji ya wenye changamoto za ulemavu ili nao wanufaike na rasilimali za taifa kama wananchi wengine wasio na ulemavu.

Wadau hao wamesema kuwa vifaa vya kusaidia wenye ulemavu kama vile vifaa vya kusaidia kuongeza usikivu, kuona, fimbo maalum za wasioona na baiskeli za miguu mitatu pamoja na vifaa vingini ni ghali kiasi kwamba mtu mwenye ulemavu si rahisi kuvipata.

Walishauri serikali iwasaidie kupata wakalimani kwa ajili ya kutafsiri habari na matukio mbalimbali kupitia Televisheni na kuwasaidia wasioona kupata CD na tepu za sauti ambazo zitawasaidia kuwafikishia habari na taarifa mbalimbali kwa wakati.

MED Hewani Kuanzia Mach 2011.

Asasi ya Marafiki wa Elimu Dodoma (MED) inatarjia kuanza kuendesha vipindi vyake vya Radio kuhusu Elimu kuanzia mwezi Machi, 2011. Wanachama wa MED na wadau wote wa Elimu wanakaribishwa kushiriki kwenye vipindi hivyo.

Hayo yameelezwa na Mratibu wa MED Bw. Davis Makundi alipkuwa akiongea na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake. Bw. Makundi amesema vipindi hivyo vitaendeshwa kwa udhamini wa mashirikaya HakiElimu na Uwezo.net yote ya jijini  Dar Es salaam                                                                                        

"Vipindi hivi vitakuwa vya moja kwa moja kutoka studio (Live) na vitaruhusu wasikilizaji walio nje ya studio kupifa simu au kutuma SMS kwa lengo la kuchangia mada au kuuliza maswali alisema" Bw. Makundi.

Vipindi hivyo vitakavyosikika kwa muda wa nusu saa (dk. 30); vitakuwa vikisika kwenye Radio Kifimbo 89.8 inayorusha matangazo yake kwenye masafa ya FM Mkoani Dodoma.            Bw. Davis Makundi