Fungua
YOUTH EDUCATION THROUGH SPORTS TANZANIA

YOUTH EDUCATION THROUGH SPORTS TANZANIA

Mbeya , Tanzania

 Mradi wa kuku mkombozi wa wanawake Singida.

In Summary

“Kipindi cha nyuma niliwahi kuhudhuria mafunzo ya ufugaji yaliyoendeshwa na Tasaf juu ya ufugaji bora na wakisasa na pia asasi ya RWDA, baada ya kuhitimu mafunzo haya sikusita kuja kuwafundisha wanakijiji wenzangu hususani wanawake na ndio maana unaona kuna mabanda mengi yanayofanana katika eneo hili” anasema mwenyekiti huyu wa UWAVYU.

 

Ni umbali wa takribani kilometa thelathini hivi, kutoka Singida mjini. Nazungumzia kijiji cha Ilongero kilichopo katika jimbo la Singida vijijini, Mkoa wa Singida.
Nikiwa njiani kuelekea huko napita kwenye mashamba makubwa ya alizeti na mtama. Mashamba haya kwa sasa yamebakiwa na mabua pamoja na majani makavu, jambo linaloashiria kuwa ni eneo lenye rutuba ambalo lina zalisha mazao mengi.
Nafanikiwa kufika Kijijini cha Ilongero majira ya saa moja usiku. Hii ilitokana na matatizo ya usafiri yaliyokuwepo baada ya serikali kupiga marufuku magari aina ya Noah, ambayo yalikuwa yakitumiwa kama vyombo vikuu vya usafiri kufikia kijiji hicho.

Asubuhi ya siku ya pili, naanza ziara yangu kwa kuzunguka maeneo mbalimbali ya kijiji hicho. Kwa msaada wa mwenyeji wangu ambaye ni mkurugenzi wa asasi ya maendeleo kwa wanawake wa vijijini RWDA, Gloria Nkungu , nafanikiwa kufika maeneo muhimu yaliyoko katika kijiji hicho.
Kama ilivyo kwa vijiji vichache nchini Tanzania ,Ilongero kimebahatika kuwa na zahanati, shule ya sekondari na shule msingi makanisa na umeme wa uhakika. Kijiji hiki kinapakana na vijiji vya Sekoture, Madamigha na Mhango.
Katika zunguka zunguka yangu navutiwa na mradi wa kuku. Sistaajabishwi na wingi wa kuku waliokuwako katika eneo hili. Kwani tangu nikiwa mdogo nilikuwa nikifahamu fika kuwa mkoa wa Singida una sifa ya ufugaji wa kuku. Jambo ambalo limechangia kwa kiasi kikubwa wafanyabiashara wengi kufika kwa ajili ya kununua kuku na kuwasafirisha mjini.
Kilichonifurahisha zaidi hadi nikavutiwa kuandika makala haya, ni namna ufugaji huo unavyofanywa katika kijiji hiki. Kwani 95% ya watu wanaojihusisha na ufugaji wa kuku ni wanawake.
Ufugaji wakuku hauitaji kutembea muda mrefu. Kwa kuwa wanawawe wengi huwa nyumbani kwa muda mwingi, hii inatosha kabisa kuwa sababu kuu ya kundi hili hujihusisha zaidi na mradi huu anasema Maria Francis mjasiriamali na mwenyekiti wa Umoja wa Waishio na Virusi Vya Ukimwi Ilongero (UWAVYU)
Anasema pia uuzaji wake ni rahisi kwani mara nyingi wateja hufika katika maeneo wanayofugia na kuuziwa kuku, ambapo bei zake ni kati y ash.5000 na 10,000.
 “Tulianzisha umoja wetu mwaka 2007. Ukiwa na wanachama wachache sana. Ingawaje kwa sasa idadi imeongezeka nafikiri ni baada ya watu wengi kupata uelewa juu ya namna ya kuishi na Virusi vya Ukimwi” anasema.
Wakati wanaanzisha umoja huo hawakuwa na mradi hata mmoja, lakini baada ya kujikusanya pamoja waliweza kuanzisha miradi hususani ya ufugaji wa kuku, kupitia msaada mkubwa wa wafadhili waliokuwa wakiupata.
“Tumekuwa tukipata ufadhili wa fedha na mafuzo kutoka katika halmashauri, Tasaf, Tagert, RWDA na mashirika mengine mengi tu jambo lililotuchochea kuufanya mradi huu wa ufugaji kwa bidii” anafafanua.
Je kupitia mradi huu mnapata faida zipi?
Kama kikundi UWAVYU wana miradi ya aina mbili. Kwanza ni mradi wa jumla ambapo wamechangia kuku kila mwanakikundi ambapo wanafuga pamoja. Na mwingine ni ule wa kila mtu kufuga mmoja nyumbani kwake.
“Licha ya kuwa na miradi mingine midogo midogo ya maendeleo, lakini naweza kusema ufugaji wa kuku tunauchukulia kama mradi mkubwa sana kwetu kwani umekuwa ukitusaidia kusomesha watoto na hata kupata mitaji ya kilimo wakati mwingine” anasema mama maria.
Baadhi ya wanakikundi wa kikundi hicho pia walimuunga mkono mwenyekiti wao wakielezea faida mbalimbali wanazopata kutokana na ufugaji wa kuku. Tatu Ismail Mkindo kutoka eneo la  Mwakiti kijijini hapo anasema ufugaji wa kuku umewasaidia sana. Kwani wakati mwingine huwa hawana haja ya kupoteza pesa kununua mbolea na badala yake hutumia kinyesi cha kuku katika mashamba yao.
“Mbali na kuuza na kujipatia lishe kwa kula nyama na mayai, tumekuwa tukipata mbolea kutokana vinyessi vyao, ambayo huchangia kwa kiasi kikubwa kuboresha mazao yetu bila kuchakaza ardhi tofauti na ile ya chumvi chumvi” anafafanua mama huyu.
Tofauti na maeneo mengine, kuku wanaofugwa katika eneo hili wanafugwa kitaalamu sana ingawaje ni wa kienyeji. Je wamepata wapi utaalamu huu?.
“Kipindi cha nyuma niliwahi kuhudhuria mafunzo ya ufugaji yaliyoendeshwa na Tasaf juu ya ufugaji bora na wakisasa na pia asasi ya RWDA, baada ya kuhitimu mafunzo haya sikusita kuja kuwafundisha wanakijiji wenzangu hususani wanawake na ndio maana unaona kuna mabanda mengi yanayofanana katika eneo hili” anasema mwenyekiti huyu wa UWAVYU.

Katika ufugaji kitu kikubwa alichojifunza ni kuwaweka kuku katika banda. Si vizuri kuwaacha na kuzagaa maeneo mbalimbali kwa kwa kufanya hivyo wanaweza kuambukizwa magonjwa kwa urahisi anasema
Kitu kingine ni ujenzi wa mabanda yenyewe. Lazima bada la kuku liwe na shemu mbili yani ile ya ndani na kwa upande wa nje kuwe na wavu ambao ni maalum kwa ajili ya kuku hao kujipatia mlo wao anaelezea.
Na pia afisa Mifugo wao aliyemtaja kwa jina moja tu la Asenga, amekuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha chanjo na masuala mengine ya kitaalamu yahusianayo na ufugaji wao huo.
Chausiku Juma kutoka Mwakiti  Ilongero, pia ni miongoni mwa wanakikundi wa UWAVYU. Anasema yeye alijifunza ufugaji kupitia kwa wanakikundi wenziwe.
Na kwa sasa amekuwa na utaalamu. Kwani kupita mradi huo ameweza kuzalisha kuku ambao kupitia wao amekuwa akiendesha maisha yake.
“Mradi wa kuku unanisaidia kulipa ada ya wanangu na pia umenifanya nisiwe tegemezi kwani naweza kujipatia fedha kwa mikono yangu mwenyewe”
Je changamoto gani wanakutana nazo katika mradi wa ufugaji kuku?
Kwa kuwa mradi huu upo wa aina mbili. Ule wa jumla na wa kujitegemea yani mtu mmoja mmoja. Kwa upande wangu sina tatizo na huu wa jumla lakini kwa ule wa mmoja changamoto kubwa ni ukosefu wa mabanda bora. Hasa ikizingatiwa kuwa wengi wetu tunaishi kwenye nyumba za matembe ( za kuezekwa kwa udongo) kwani mara nyingine huwa ni rahisi kuvuja na hivyo kuathiri ufugaji anasema Amina Shaabani moja wa wanakikundi
Akizungumzia mipango yao ya baadaye Mama Maria Francis anasema wanalenga kununua mashine ya kutotoleshea vifaranga. Kwani kupitia hiyo tutaweza kuuza vifaranga wengi zaidi na hivyo kuzidi kujiingizia pato.
Wito wetu kwa serikali ni kupeleka miradi zaidi kwa walioathiriwa na Virusi vya ukimwi. Kwani wakijimudu kiuchumi wataweza kuishi maisha yenye furaha zaidi na hivyo kutoa mchango kwa jamii inayowazunguka.
“Ukimwi sio ulemavu wa kumfanya mtu ashindwe kushiri shughuli za maendeleo” wanahitimisha

29 Oktoba, 2012
« Iliyotangulia Ifuatayo »

Ongeza maoni

Jina lako:
Mahali ulipo:
Email yako:
(sio lazima)
Anwani yako ya email haitachapishwa.