Niache Nisome; kampeni ya kuwakomboa wasichana kielimu Handeni.
TAFITI kadhaa na hata uzoefu vinaonyesha kuwapo kwa idadi kubwa ya watoto wa kike wanaokosa fursa za elimu nchini.
Sababu zinazochangia hali hiyo ni nyingi, lakini zilizo maarufu ni pamoja na wazazi kukataa makusudi kusomesha wasichana kwa madai kuwa hawana tija hata wakisoma, wasichana kulazimishwa kuolewa wakiwa wagali wadogo na kupata ujauzito.
Kwa mfano, utafiti wa masuala ya demografia wa mwaka 2005, unaonyesha kuwa asilimia 30 ya watoto wenye umri wa miaka 15 hadi 18 wameolewa nchini, ikilinganishwa na asilimia 0.9 ya wanaume wenye umri huo waliooa.
Aidha, takwimu kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, zinasema mwaka 2011 pekee, kesi za wanafunzi kulazimishwa kuolewa katika visiwa vya Unguja na Pemba zilikuwa 32.
Takwimu hizo ni za sehemu moja tu katika nchi inayotajwa kuwa na idadi kubwa ya watoto wa kike wanaokosa fursa za kielimu kwa sababu na visingizio mbalimbali.
Hata hivyo, wapo wadau wa elimu walioamua kulivalia njuga suala hili, kwa lengo la kuhakikisha watoto wa kike nchini wanasoma, kuelimika na hatimaye kujikomboa kimaisha.
Mfano mzuri ni wadau wa elimu katika wilaya ya Handeni, mojawapo ya maeneo yanayotajwa kuwa na idadi kubwa ya watoto wa kike wanaokosa fursa za kielimu kwa sababu kadhaa, ikiwamo ndoa za utotoni na kupata mimba.
Kuhusu mimba, Jeshi la Polisi wilayani humo linasema tatizo ni kubwa na limekuwa likiwaathiri wanafunzi wengi hasa katika maeneo yenye idadi kubwa ya watu kama vile vijiji vya Kwachanga, Misima, Kabuku, Mkata na Chanika.
“Kwa mujibu wa kesi zilizoripotiwa katika vituo vya Polisi vya Mkata, Kabuku na Handeni, tatizo la mimba kwa wanafunzi wa kike ni kubwa zaidi kwa wanafunzi wa sekondari kuliko wa shule za msingi,’’anasema Mkuu wa Upelelezi wa Handeni, J. Jumanne.
Niache Nisome
Bila shaka kushamiri kwa matukio ya mimba Handeni na ongezeko la wasichana wanaoacha masomo, kumewastua wadau ambao kwa kupitia ofisi ya wilaya, wameamua kuanzisha kampeni maalumu ijulikanayo kwa jina la ‘’Niache Nisome inayopigia chapuo uboreshaji wa mazingira ya elimu kwa watoto wa kike.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni na kinara wa kampeni hiyo, Muhingo Rweyemamu, anasema kampeni ya Niache nisome inabeba ujumbe wa kuwatia ujasiri wanafunzi wa kike kuweza kuwa na sauti ya kishujaa yenye lengo la kumkomboa kielimu.
Aidha, ujumbe huo anasema unamwezesha mtoto wa kike kujitetea mwenyewe ili kuweza kufikia malengo aliyojiwekea.
Anaeleza kuwa kampeni hiyo ambayo pia inahusu jamii kwa jumla inalenga kumwezesha mtoto wa kike
kufikia malengo yanayomhusu kimaendeleo kama mwanadamu.
“ Kampeni inapanga kuweka bayana matatizo ya uwiano wa kijinsia na ukiukwaji haki za mtoto wa kike kwa kutumia mbinu za kujithamini…’’anasema Muhingo ambaye tangu achaguliwe kuiongoza wilaya hiyo amejipambanua kama mpiganaji wa haki za wasichana kielimu.
Kwa mujibu wa Rweyemamu, tatizo la watoto kukatisha masomo kwa sababu ya ujauzito ni kubwa, na kama halitotafutiwa ufumbuzi itakuwa muhali kuvunja anachokiita mduara wa umaskini kwa watoto wenyewe, familia, jamii na taifa kwa jumla.
Kuhusu shughuli zitakazoipamba kampeni hiyo, anaeleza kuwa ni pamoja na kuboresha mazingira, kuendesha vipindi vya malezi, kuandaa vitini vya taarifa kuhusu ukuaji, utetezi, ushauri-nasihi na kuendesha majukwa ya wasichana na wavulana.
Mbali ya kuwa na jamii yenye mtazamo chanya kuhusu suala la elimu kwa mtoto wa kike na hatimaye kumpa ulinzi na utetezi, kampeni hiyo anasema itawawezesha walengwa kujiamini, kuwa na uwezo wa kujitetea, kuthamini na kuimiliki miili yao na kuwa na uwezo wa kufanya uamuzi sahihi.
Wadau wakutana
Kuonyesha dhamira yao ya kumkomboa mtoto wa kike, wadau mbalimbali wa elimu wilayani humo walikutana Oktoba 11 kujadili mustakbali wa elimu kwa wasichana wa Handeni.
Akifungua majadiliano ya wadau hao yaliyofanyika sambamba na maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Chiku Galawa alisema ni muhimu kuwapa watoto wa kike elimu, kwa kuwa ndio chanzo cha maendeleo ambayo aghlabu huanzia katika ngazi ya familia.
“ Wazazi waelimishwe kuhusu athari za kuzuia watoto kusoma, bila elimu hatuwezi kujitambua,’’alisema na kuongeza:
“Rasilimali za Handeni zinahitaji watu walioelimika, wakiwamo wanawake watakaoelimika kupitia kusoma. Bila elimu rasilimali hizo zitachezewa.’’
Katika mkutano huo wa majadiliano, wadau pamoja na mambo mengine walishauri kufanyika kwa mazoezi ya upimaji mimba shuleni mara kwa mara na kuendelea kuhamasisha jamii kuthamini elimu kwa mtoto wa kike.
Ukitoa ofisi ya Mkuu wa Wilaya inayoratibu kampeni, mdau mwingine mkuu wa kampeni hiyo ni shirika la Elimu Duniani maarufu kwa kifupi cha WEI, kupitia mradi wa Pamoja tuwalee unaofadhiliwa na Shirika la Misaada la Marekani (USAID).