Fungua
The Foundation for Human Health Society.

The Foundation for Human Health Society.

KAHAMA, Tanzania

DKT. BITEKO AZINDUA TEKNOLOJIA YA KUONDOA UVIMBE MWILINI BILA UPASUAJI

1000755915.jpg



πŸ“Œ Ni kwa mara ya kwanza kufanyika Afrika Mashariki na Kati


πŸ“Œ Aipa kongole Hospitali ya Kairuki kwa kutoa punguzo la asilimia 50 kwa wagonjwa 50 wa kwanza


πŸ“Œ Asema Serikali itaendelea kuweka msukumo ushirikiano na Sekta binafsi


πŸ“Œ Awaasa Watendaji Wizara ya Afya kutoogopa kujifunza pale Sekta binafsi inapofanya vizuri


πŸ“Œ Wagonjwa 300 wanufaika na teknolojia ya utoaji uvimbe bila upasuaji


Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameziindua teknolojia ya kuondoa uvimbe mwilini bila upasuaji inayofahamika kama High-Intensity Focused Ultrasound (HIFU) katika Hospitali ya Kairuki ikiwa ni mara ya kwanza kwa huduma hiyo kuzinduliwa katika nchi za Afrika Mashariki na Kati.


Akizindua huduma hiyo Agosti 27, 2025 jijini Dar es Salaam, Dkt. Biteko amepongeza Watendaji wa hospitali ya Kairuki pamoja na muasisi wake Hubert Kairuki na Mkewe kwa uthubutu wao katika masuala mbalimbali ikiwemo utoajiwa huduma hiyo ya HIFU ambayo imeiweka Tanzania katika rekodi ya kutoa uvimbe bila kufanya upasuaji barani Afrika suala ambalo pia litaongezea nchi mapato.


Ameeleza kuwa awali huduma ya HIFU barani Afrika likuwa ikipatikana katika nchi tatu tu ambazo ni Misri, Nigeria na Afrika Kusini.


Aidha, ameipongeza Hospitali ya Kairuki kwa kutoa punguzo la asilimia 50 la gharama za matibabu ya utoaji uvimbe bila upasuaji kwa wagonjwa 50 wa kwanza ndani ya kipindi cha mwezi mmoja kuanzia leo ikiwa ni kielelezo cha Watendaji wa hospitali hiyo kuonesha utu kwa Watanzania, kuacha alama njema na kuunga mkono dhamira ya Serikali ya kutoa huduma kwa watanzania kwa gharama nafuu.


Dkt. Biteko amesema kuwa kufanyika kwa tukio hilo muhimu ni kielelezo cha Serikali ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuipa msukumo sekta binafsi na kuikuza ili kutoa huduma za matibabu kwa wananchi kwa ufanisi na kusogeza karibu huduma ambazo hapo awali zilikuwa hazipatikani ndani ya nchi hivyo ameahidi kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono Sekta binafsi.


Β·Aidha, ameipongeza Hospitali ya Kairuki kwa kuanzisha Idara ya huduma za dharura ambayo ina uwezo wa kuhudumia wagonjwa zaidi ya 9,000 kwa mwaka.


Katika hatua, nyingine, Dkt. Biteko amewataka Watendaji katika Wizara ya Afya kutoogopa kujifunza kutoka Sekta binafsi pale inapofanya vizuri na wawape ushirikiano wakati wote siyo nyakati za ukaguzi tu kwani lengo la Serikali ni kufikisha huduma bora kwa wananchi kwa ushirikiano wa Serikali na sekta hiyo.


Kuhusu ombi la Hospitali ya Kairuki la kujengewa barabara ya lami ya mita 300 kuelekea kwenye hospitali hiyo ili kurahisisha utoaji huduma kwa wananchi ameelekeza Manispaa ya Kinondoni kufanyia kazi ombi hilo.


Dkt. Mwinyikondo Amir, kutoka Wizara ya Afya akimwakilisha Waziri wa Afya, amesema kuwa tukio hilo ni ishara ya ushirikiano uliopo kati ya sekta binafsi na Serikali katika kutoa huduma bora kwa wananchi.


Amesema Wizara ya Afya imekuwa na ushirikiano mkubwa na Hospitali ya Kairuki katika masuala mengi ikiwemo matumizi ya Bima ya Afya na kwamba pande zote mbili zinatambua kuwa zina wajibu wa kutekeleza dira ya maendeleo ya 2050 inayoelekeza uwepo wa jamii yenye afya bora.


Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Afya na Elimu Kairuki, Kokushubila Kairuki ameishukuru Serikali kwa kutambua mchango wa sekta binafsi katika kuboresha huduma za afya nchini.


Amesema sekta ya afya imekuwa na maendeleo makubwa chini ya uongozi wa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan na kwamba hospitali hiyo itaendelea kuunga mkono juhudi hizo hasa ikiwa ni utekelezaji wa Dira 2050 inayolenga kujenga Taifa lenye uchumi imara na afya bora.


Amesema gharama za kuweka teknolojia hiyo ya HIFU ni shilingi Bilioni 12 na milioni 300.


Aidha amesema kutoka huduma ya HIFU ianze kutolewa tayari wananchi 300 wamepata huduma za uchunguzi huku 298 wakipata matibabu.


Awali, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Kairuki,Β Dk. Onesmo Kaganda alisema uzinduzi wa HIFU ni tukio la kihistoria kwakuwa ni mara ya kwanza kwa huduma hiyo kuzinduliwa katika nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.


Amesema teknolojia hiyo barani Afrika imeanzishwa katika nchi tatu tu ambazo ni Misri, Nigeria na Afrika Kusini.


Ameeleza kuwa HIFU ni Teknolojia ya kisasa inayotumia Mawimbi Sauti (Sound Waves) b kutibu aina mbalimbali za uvimbe mwilini bila upasuaji, ikiwemo uvimbe wa saratani na usiokuwa wa saratani katika maeneo kama Matiti, Kongosho, Kizazi kwa Wanawake, na Tezi Dume kwa wanaume.


Ameeleza faida za huduma hiyo kuwa ni pamoja na kutokuwa na kovu kwa kuwa hakuna upasuaji, mgonjwa hawekewi nusu kaputi na mgonjwa hupona kwa muda mfupi na kurejea katika shughuli zake, matibabu hayahitaji kumwongezea damu mgonjwa hata kwa wagonjwa wenye upungufu wa damu, pia kupunguza gharama za kwenda nje ya nchi kutafuta matibabu.


Ameongeza kuwa, faida nyingine ya HIFU ni pamoja na tiba shufaa ambayo husaidia dawa za saratani kufanyakazi vizuri mwilini, kufubaza kukua kwa saratani mwilini (slowdown disease progression) na kupunguza maumivu kwa wagonjwa wa saratani.


Amesema mtambo huo ulianza kufanya kazi desemba 2023 ambapo mpaka sasa wagonjwa 303 wamefanyiwa uchunguzi na 298 kupatiwa matibabu na kumekuwa na matokeo chanya ya wagonjwa hao.


Amesema kuwepo kwa teknolojia hiyo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya za kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha utalii Tiba Kusini mwa jangwa la Sahara.


Pia, amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuweka mazingira wezeshi ya ushirikiano kati ya Serikali na Taasisi Binafsi.


Kuhusu Idara ya Huduma za Dharura iliyozinduliwa katika Hospitali ya Kairuki amesema itakuwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa zaidi ya 9000 kwa mwaka na pia imejizatiti kwa magonjwa ya dharura pindi yatakapotokea.


Mwisho
1000755915.jpg
1000755914.jpg
1000755916.jpg
1000755917.jpg
1000755918.jpg
1000755919.jpg
1000755920.jpg
1000755921.jpg
1000755922.jpg
1000755924.jpg
1000755923.jpg
1000755925.jpg
1000755926.jpg
1000755927.jpg
1000755928.jpg

MGOMBEA UDIWANI KATA YA NGOGWA ABEL MABAO AREJESHA FOMU




1000756741.jpg


Mgombea udiwani wa Kata ya Ngogwa kupitia chama cha mapinduzi (CCM) Abel Mabao,Β  agosti 27, 2025 ameweka historia baada ya kurejesha fomu za kugombea nafasi hiyo katika ofisi za kata hiyo.

Mabao, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mabao Investment, amewasili katika ofisi za kata akiwa na wafuasi wake na kupokelewa na mtendaji wa kata Pendo Shirima ambaye amepokea fomu hizo kwa mujibu wa taratibu za uchaguzi.

Akizungumza mara baada ya kurejesha fomu, Mabao ameshukuru wafuasi wake na wananchi wa Ngogwa kwa mshikamano waliomuonesha, akiahidi kampeni zenye maadili na kujikita katika maendeleo ya jamii.

Zoezi la urejeshaji fomu za wagombea udiwani limetamatika leo nchini kwa mujibu wa ratiba ya uchaguzi.


1000756742.jpg
1000756752.jpg
1000756749.jpg
1000756741.jpg
1000756735.jpg
1000756737.jpg
1000756744.jpg
1000756732.jpg
1000756761.jpg
1000756759.jpg
1000756718.jpg
1000756721.jpg


KAILIMA AFUNGA KIKAO CHA UPANGAJI WA RATIBA YA KAMPENI ZA WAGOMBEA URAIS


INEC3266.jpg

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) Ndugu Kailima R.K, amefunga kikao cha siku mbili cha Tume na Vyama vya Siasa 18 vyenye usajili kamili na ambavyo vimependekeza wagombea wa kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makamu wa Rais, kwa lengo la kujadili na kupanga kwa pamoja ratiba ya kampeni za vyama hivyo.


Kikao hicho kilichoketi Agosti 25 na 26, 2025 kilishirikisha vyama vya Civic United Front (CUF), National Convention for Construction and Reform (NCCR-Mageuzi), Union for Multiparty Democracy (UMD), Chama cha Mapinduzi (CCM), National League for Democracy (NLD), United Peoples’ Democratic Party (UPDP) na National Reconstruction Alliance (NRA), African Democratic Alliance Party (ADA-TADEA).

Vyama vingine ni Tanzania Labour Party (TLP), United Democratic Party (UDP), Madini Kilimo Nishati (MAKINI), Democratic Party (DP), Sauti ya Umma (SAU), Alliance for African Farmers Party (AAFP), Chama cha Kijamii (CCK), Alliance for Democratic Change (ADC),Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) na Alliance for Change and Transparency (ACT-Wazalendo).


Kampeni za Uchaguzi zinatarajiwa kuanza Agosti 28, 2025 hadi Oktoba 28, 2025 nchini kote ambapo wagombea watakaoteuliwa na Tume watafanya kampeni za kunadi sera za vyama vyao kutafuta ridhaa ya wananchi kuwapigia kura Oktoba 29, 2025 katika uchaguzi mkuu.
INEC3262.jpg

INEC3255.jpg

INEC3254.jpg
INEC3278.jpg


INEC3273.jpg

DKT. DOTO BITEKO ACHUKUA FOMU KUGOMBEA UBUNGE JIMBO LA BUKOMBE





πŸ“Œ Wanachama zaidi ya 1000 wajitokeza kumdhamini




πŸ“Œ Dkt. Biteko ahimiza Kampeni za kistaarabu, mshikamano na upendo




πŸ“Œ Awaomba Wana Bukombe kumchagua Dkt. Samia, Biteko na madiwani wa CCM




Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati




Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Bukombe, Zedekiah Solomon Osan amemkabidhi fomu ya uteuzi wa kugombea nafasi ya Ubunge wa Jimbo la Bukombe kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Doto Mashaka Biteko leo Agosti 26, 2025 katika Ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Bukombe - Mkoani Geita.




Makabidhiano hayo ya fomu ni utekelezaji wa ratiba kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29 mwaka 2025 Aidha, Maelefu ya wana CCM na wapenzi wa chama hicho wamemsindikiza mgombea kwa ajili ya kuchukua fomu kwa ajili ya kuomba kuteuliwa na Tume huru ya Uchaguzi.




Katika hali isiyo ya kawaida, zaidi ya wanama 1000 wamejotokeza kumdhamini Dkt. Biteko ikilinganishwa na mahitaji ya wadhamini 31 waliohitajika kisheria.




Akizungumza na wanaCCM katika viwanja Ofisi ya CCM Wilaya ya Bukombe, Dkt. Biteko amewataka wananchi kudumisha mshikamano na upendo miongoni mwao na kuwachagua viobgozi bora.




β€œ Utakapofika wakati tuwaxhague viongozi tunaowapenda, nawaomba mmchague Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Rais, Mnichague mimi kuwa mbunge na niwaaombe mbiletee madiwani wa CCM kwa tuendeleze kazi tuliyokwisha ianza,”




Awali, Katibu wa CCM, Wilaya Bukombe Leonard Mwakalukwa amesema wana CCM zaidi ya 3500 wamejitokeza kumsindikiza mgombea katika Ofisi za tume huru ya Uchaguzi kwa ajili ya kuchukua fomu.




Amesema wadhamini 31 kutoka Kata zote 17 za Bukombe wamewawakilisha wenzao 969 waliojitokeza kumdhamini mgombea.




MWISHO

DKT. BITEKO AHIMIZA UTEKELEZAJI WA MAAZIMIO VIKAO VYA KIMKAKATI VYA WENYEVITI WA BODI NA WAKUU WA TAASISI

1000752480.jpg
1000752479.jpg
1000752478.jpg
1000752481.jpg
1000752484.jpg
1000752485.jpg

πŸ“Œ Awakumbusha kuhusu dhamana waliyobeba ya kubadili maisha ya watanzania kupitia mtaji wa shilingi Trilioni 86 waliopewa


πŸ“Œ Afunga Kikao kazi cha Tatu cha Wenyeviti wa Bodi, Wakuu wa Taasisi


πŸ“Œ Asema Rais, Dkt. Samia anatambua mchango wa Taasisi za umma; ana matarajio makubwa kutoka kwao


πŸ“Œ Awakumbusha kutekeleza Maagizo yaliyotolewa na Makamu wa Rais


πŸ“Œ Kikao kazi chafanyika kwa mafanikio; chahusisha washiriki zaidi ya 600


Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewahimiza Wenyeviti na Wakuu wa Taasisi za Umma nchini kusimamia utekelezaji wa maazimio ya kimkakati yanayofikiwa katika vikao kazi wanavyofanya kwa kutambua kuwa wamebeba dhamana ya kuboresha maisha ya Watanzania kupitia mtaji wa shilingi Trilioni 86 ambao Serikali imewekeza kwenye Taasisi na mashirika yake..


Dkt. Biteko ameyasema hayo tarehe 26 Agosti 2025 jijini Arusha wakati akifunga kikao kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma (CEOs FORUM 2025).


β€œWatanzania wanawategemea ninyi kuwabadilishia maisha, kama tunazungumza kuhusu umaskini wa watu, Serikali inapaswa kuwa kiongozi wa kuwaondolea watu umaskini wao, hivyo hamna budi kutambua kuwa mnalo deni la kuboresha hali zetu na maisha yetu.” Amesema Dkt. Biteko


Dkt. Biteko amewahakikishia Watendaji hao kuwa Serikali katika ngazi zote inatambua mchango wa taasisi na mashirika katika ukuaji wa uchumi na pia inatambua mchango wa vikao kazi vya watendaji hao ambavyo vimepelekea mashirika kuongeza mchango wake katika mfuko mkuu wa Taifa.


" Vikao kazi hivi mnavyofanya vimeonesha mchango wake katika uchumi, mfano katika kikao kazi cha mwaka 2024 mliazimia mashirika ya umma yaboreshe utendaji na kuongeza uchangiaji katika mfuko mkuu wa Serikali na matokeo yameonekana mfano Shirika la Maendeleo ya Petroli ( TPDC) liliongeza uchangiaji wake kwa asilimia 100, shirika hili liliongeza uchangiaji wake kutoka shilingi bilioni 5.5 kwa mwaka 2023/2024 hadi shilingi bilioni 11.1 mwaka 2024/2025." Amesema Dkt.Biteko


Ameongeza kuwa, uchagiaji wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) umeongezeka kwa asilimia 363 katika mfuko mkuu wa Serikali ambapo NHC ilichangia shilingi bilioni 1.2 mwaka 2023/ 24 na mwaka 2024/2025 ilichangia shilingi bilioni 5.5.


Dkt. Biteko amewaeleza Wenyeviti wa Bodi na Wakuu wa Taasisi kuwa β€œRais Samia pamoja na kuthamini mchango wenu kwa Serikali anatarajia mengi kutoka kwenu na Watanzania wana matarajio makubwa hasa wakati tukielekea kwenye utekelezaji wa Dira 2050, endeleeni kuongeza mchango wenu kwenye ukuaji wa uchumi, mjitegemee na muwe mfano wa taasisi binafsi."


Katika.hatua nyingine, Dkt. Biteko ametaka viongozi hao kufanyia kazi agizo lililotolewa na Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango la kudhibiti mianya ya uvujaji wa mapato.


Pia amempongeza Msajili wa Hazina kwa kuwa na maono ya kuratibu kikao kazi hicho ili kujadili masuala yatakayosukuma mbele utendaji wa taasisi.


Katika hafla hiyo, Dkt. Biteko hakuacha kukumbusha kuhusu ushiriki wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 ambapo amesema uchaguzi huo uwe ni ajenda ya watu wote wakiwemo Wenyeviti wa Bodi na Wakuu wa Taasisi hivyo waone kuwa wana wajibu wa kuwasisitiza watu kwenye taasisi zao kujitokeza kusikiliza wagombea na baadaye kupiga kura kwa amani kwani kukiwa na amani mashirika hayo pia yatafanya vizuri zaidi.


Naibu Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Mhe. Stanslaus Nyongo kwa upande wake, amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa dira na muongozo katika kuendeleza mashirika ya umma ili yaweze kuwa na tija nchini.


Amesema katika siku tatu za kikao kazi washiriki wamejifunza na kubadilishana uzoefu kupitia watoa mada wa ndani na nje ya nchi waliobobea.


Amesema Wizara ya Mipango na Uwekezaji itahakikisha maazimio ya kikao kazi hicho yanatekelezwa ipasavyo, pia Wizara itasimamia mageuzi ya kuhakikisha mashirika ya umma yanachangia ukuaji wa pato la taifa hadi kufikia Dola za Marekani trilioni 1 ifikapo 2050 ambapo kwa sasa pato la taifa ni dola za Marekani bilioni 85.


Kwa upande wake Salim Kali, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Arusha amesema wilaya 6 za Mkoa wa Arusha zimefikiwa na umeme hadi ngazi ya vijiji, pia miradi ya maji imefanyika pamoja na miundombinu ya Barabara ambayo imewezesha maisha bora kwa watu wa aina zote wakiwemo watalii.


Awali, Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu alisema kuwa katika kikao kazi hicho kampuni zaidi 300 zimeshiriki huku washiriki wakiwa ni zaidi ya 650.


Alisema kikao kilikuwa na majadiliano mbalimbali ya kina yanayolenga kusukuma mbele uchumi wa nchi na kusimamia uwekezaji wa Serikali kwa taasisi za umma wa zaidi ya shilingi trilioni 86.


Mkutano huo wa Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma uliongozwa na kaulimbiu ya "Ushirikiano Endelevu wa Kibiashara katika Mazingira Shindani Kimataifa - Nafasi ya Mashirika ya Umma."


Mwisho

AHADI YA SERIKALI KUFIKISHA UMEME WA GRIDI KAGERA YATEKELEZWA

1000749074.jpg
1000749075.jpg
1000749076.jpg
1000749077.jpg
1000749078.jpg
1000749079.jpg
1000749080.jpg
1000749081.jpg
1000749082.jpg
1000749083.jpg



πŸ“Œ Dkt.Biteko ashuhudia utiaji saini mikataba itakayowezesha Wilaya zote Kagera kupata umeme wa Gridi


πŸ“Œ Awali umeme mwingi ulikuwa ukitoka nchini Uganda hivyo kufanya Mkoa kutokuwa na umeme wa uhakika na wa kutosha


πŸ“Œ Asema Rais.Dkt. Samia alishatoa maagizo ya mradi huo kutekelezwa kwa wakati na kwa usahihi


πŸ“Œ Aagiza wananchi 1,014 waliopisha mradi kulipwa fidia kuanzia mwezi Septemba 2025



πŸ“Œ Apongeza Wizara ya Nishati na TANESCO kwa ufanisi katika.usimamizi wa miradi



Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati




Ahadi ya Serikali ya kufikisha umeme wa gridi ya taifa katika Wilaya zote za Mkoa wa Kagera imetekelezwa baada ya Serikali kusaini mikataba ya ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 220 kutoka Benako, Ngara hadi Kyaka wilayani Misenyi na kituo cha kupoza umeme cha Benako cha msongo wa kilovoti 220/33, hatua inayotoa uhakika kwa Mkoa huo sasa kupata umeme wa gridi badala ya kutegemea umeme kutoka Uganda kwa kiasi kikubwa.


Akizungumza baada ya kushuhudia utiaji saini kwa mikataba hiyo jijini Dodoma tarehe 25 Agosti, 2025, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa kuanza kutekelezwa kwa mradi huo ni moja ya maelekezo ya Dkt.Samia Suluhu Hassan ambaye alikuwa na kiu ya kutekeleza ahadi ya Serikali kwa wananchi wa Kagera ya kupata umeme wa uhakika muda wote ili kutekeleza shughuli zao za kiuchumi na kijamii.


" Kupitia mradi huu, Mkoa wa Kagera kwa mara ya kwanza na wenyewe unaingia kwenye gridi ya Taifa hasa na hivyo kuongeza uhakika wa upatikanaji wa umeme hususan katika Wilaya za Bukoba, Muleba, Misenyi, Karagwe, Kyerwa na maeneo mengine ya jirani, nawahakikishia watu wa Kagera kuwa Serikali imeshaamua mradi huu ufanyike kwa wakati kwa miezi 24 tu" Amesema Dkt. Biteko


Dkt. Biteko amesema, Kagera ambayo mahitaji yake ya umeme hayazidi megawati 47 baada ya muda itakuwa na uhakika mkubwa wa upatikanaji umeme kwani kutakuwa na njia mbalimbali za kufikisha umeme mkoani humo ikiwemo Benako- Karagwe hadi Kayaka, Nyakanazi- Biharamulo hadi Muleba na kuna mradi mwingine mkubwa unaotarajiwa kujengwa kutoka Ibadakuli hadi Mbarara Uganda wa kV 400. Vilevile kuna mradi wa uzalishaji umeme wa Kakono wa megawati 87 ambao upo katika hatua za mwisho za kutafuta Mkandarasi.


Ameongeza kuwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan pia anaendelea kutekeleza miradi mingine ya umeme katika maeneo mengine ikiwemo mradi wa usafirishaji umeme wa kV 400 wa Tanzania- Zambia, mradi wa Usafirishaji umeme wa kV 400 Chalinze-Dodoma , mradi wa usafirishaji umeme wa Mkuranga -Pwani ambao utapeleka umeme kwa wananchi wa Kusini, pia mradi wa usafirishaji umeme wa gridi imara wa Tunduru- Masasi- Mahumbika ambao pia unaenda kutoa uhakika wa umeme katika mikoa ya Kusini.


" Utekelezaji wa miradi hii yote ya umeme ni kielelezo kuwa, Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshaonesha njia ya kuwafikishia wananchi umeme wa uhakika sasa kinachohitajika kwa watendaji ni kukimbia badala ya kutembea kwani kinachotakiwa ni matokeo na siyo kusema sana." Amesisitiza Dkt. Biteko


Pia Dkt. Biteko amewashukuru wafadhili wa mradi ambao wametoa Dola za Kimarekani takriban milioni 105.6 ambazo ameagiza kuwa zitumike kwa usahihi ili kuwapa sababu wafadhili wengine kuendelea kusaidia miradi mbalimbali.


Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko ameagiza TANESCO kuhakikisha wananchi 1,014 wanaopisha mradi wanalipwa fidia yao mapema iwezekanavyo yaani kuanzia mwezi septemba mwaka huu.


Aidha, amempongeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga na watendaji wa TANESCO kwa kuendelea kusimamia kwa umakini Sekta ya Nishati.


Vilevile, ameipongeza TANESCO kwa kuendelea kuboresha utendaji wake na kwa kusimamia haki hasa pale zabuni zinapotangazwa. Aidha ametaka mipango iliyowekwa kwenye mradi huo iheshimiwe ili thamani ya fedha ionekane na wananchi wapate huduma kwa wakati.


Dkt. Biteko ameomba wananchi mkoani Kagera kuchangamkia fursa kutokana na kuwepo kwa umeme wa uhakika mara baada ya miradi itakayofikisha umeme mkoani humo kukamilika.


Naye Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatuma Mwassa amepongeza Serikali kwa kuona umuhimu wa kutekekeza mradi huo wenye gharama kubwa ikiwa ni kuonesha kwa vitendo jinsi inavyowajali wananchi hao.


Amesema wilaya zote mkoani Kagera zitaunganishwa na gridi kwani kwa sasa no wilaya tatu tu ndio zimeunganishwa na Gridi ya Taifa.


Ameahidi kuwa, Wananchi katika mkoa huo watakuwa watumiaji wazuri wa umeme na walipaji bili wazuri iili TANESCO iendelee kupata mapato ya kutekeleza miradi mingine l.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amesema Mkoa wa Kagera ni miongoni mwa mikoa minne ambayo haijaunganishwa kwenye gridi ya Taifa ikiwemo Rukwa, Lindi na Mtwara.


Amesema tukio la leo ni la kihistoria kwani kukamilika kusainiwa kwa mikataba hiyo kunafanya mikoa yote iliyo nje ya gridi kuwa kwenye mpango wa kupelekewa umeme gridi hivyo kwa sasa hakuna mkoa ulio nje ya gridi ambao hauna mradi wa kupelekewa umeme.


Amesema kwa sasa Mkoa wa Kagera unapata umeme wa megawati 40 kutoka nchini Uganda kupitia kituo cha Kyaka na megawati 7 kutoka mwekezaji binafsi wa mradi wa Mirongo/ Kikagati.


Amesema wakati Serikali ya Awamu ya Sita inaingia madarakani jumla ya mikoa sita kati ya 26 haikuwa imeunganishwa kwenye gridi ya Taifa ila kwa kipindi cha minne Serikali imefanikiwa kuunganisha umeme Kigoma na Katavi huku mingine iiliyosalia ikiwa miaradi inayoendelea kutekekelezwa.


Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania ( TANZANIA), Lazaro Twange mradi huo una umuhimu mkubwa mkoani Kagera kwani wilaya za Kyerwa, Karagwe, Misenyi, Muleba, Bukoba Vijijini na Manispaa ya Bukoba kwa muda mrefu sasa zimekuwa zikiitumia umeme kutoka nchini Uganda takribani megawati 40 kupitia kituo cha kupoza umeme cha Kyaka ambacho kinapokea umeme kutoka Masaka, Uganda kupitia njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 132 kufuatia mkataba wa makubaliano baina ya Tanzania na Uganda.



Pia, kukamilika kwa mradi huo kutawezesha kuunganishwa kwa kituo cha kuzalisha umeme cha Kakono katika Gridi ya Taifa.



Amesema gharama za mradi ni shilingi bilioni 262.5 na utatekelezwa kwa muda wa miezi 24.


Amesema.Mradi huu unatekelezwa kwa fedha za Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo ambapo Mfuko wa Maendeleo wa Shirika la Wauzaji Mafuta Duniani (OPEC) utachangia dola za Marekani milioni 60, Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi utachangia dola za Marekani milioni 30, Mfuko wa Maendeleo wa Saudia utachangia dola za Marekani milioni 13 na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itachangia dola za Marekani milioni 2.6 kwa ajili ya fidia kwa wananchi watakaopisha mradi.


Amesema Wakandarasi watakaotekeleza mradi huo ni kampuni ya M/s. TBEA Co. Ltd kutoka nchini China ambayo itahusika na ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Benako, na Kampuni ya M/s. Transrail Lighting Limited kutoka India itahusika na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Benako hadi Kyaka.